Katika hatua ya kijasiri ya kuvutia walimu na wachungaji wapya wenye sifa, Konferensi ya Yunioni ya Lake nchini Marekani inatoa ahadi ya dola milioni moja za Marekani kwa wanafunzi wapya wa Chuo Kikuu cha Andrews ili wafuate taaluma katika ualimu na huduma ya uchungaji.
Kuanzia muhula wa masomo wa msimu wa vuli 2024, ufadhili utagharamia miaka minne ya masomo katika mojawapo ya fani hizi mbili.
Kuendesha mpango huu ni kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaofuatilia kazi za umuhimu mkubwa kwa kanisa. “Tunaona haja halisi ya kuajiri walimu na wachungaji zaidi,” alisema Ken Denslow, rais wa Konferensi ya Yunioni ya Lake. “Kadri walimu wanavyohamia au kustaafu, tunaona ni vigumu zaidi kujaza nafasi hizi. Kuna vijana ambao wangekuwa tayari kuitikia wito wa kuwa walimu na wachungaji, lakini gharama inakuwa kikwazo.”
Ruth Horton, mkurugenzi wa elimu wa Yunioni ya Lake, ameshuhudia kupungua kwa idadi ya walimu wanaopatikana. “Mwaka ujao wa shule, tunatarajia nafasi kadhaa za walimu katika shule zetu za Utotoni hadi Daraja la 12,” alisema. “Kwa wakati huu, hakuna wanafunzi wa kutosha wanaohitimu kutoka Chuo Kikuu cha Andrews kujaza nafasi zilizopo na zile tunazotarajia katika siku za karibuni.”
Ingawa idadi ya nafasi za uchungaji katika Yunioni ya Lake si kubwa kwa sasa, kadri wachungaji wanavyostaafu, Divisheni ya Amerika Kaskazini inatabiri hadi nafasi 2,000 kote katika divisheni hiyo katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Uongozi wa idara unajihusisha katika kukabiliana na mgogoro unaonyemelea.
Mbali na kustaafu, ukuaji mkubwa wa idadi ya wahamiaji na wakimbizi katika eneo la Yunioni ya Lake na zaidi unaunda fursa ya kuwafunza wale walioitwa kuhudumia makundi haya, alisema Carmelo Mercado, makamu wa rais wa wa huduma za kitamaduni wa Yunioni ya Lake . “Vijana wengi wetu wana nia ya kuhudumu kanisani, lakini kama wanafunzi wa kizazi cha kwanza hawana rasilimali za kuhudhuria vyuo vyetu vikuu,” alisema Mercado. “Hii itakuwa baraka kwao.”
Kamati ya uongozi inayojumuisha viongozi wa yunioni, konferensi, na vyuo vikuu inaanzisha vigezo vya kutoa ufadhili. Maelezo zaidi yanatarajiwa katika wiki zijazo. Yunioni ya Lake inaungana na yunioni zingine kadhaa katika kutoa ufadhili kwa wachungaji na walimu wanaochipukia.
Wasimamizi wa Yunioni ya Lake walisema wanatumai mpango huu utachochea washiiki wa kanisa kuwekeza zaidi katika viongozi wa baadaye. “Hii ni mpango wa imani,” alisema Glynn Scott, mweka hazina wa Yunioni ya Lake. Maeneo mengine yalitumia zawadi maalum za mfuko wa amana, lakini sisi tunatumia akiba yetu. Hata hivyo, tunaamini Mungu atatubariki tunapojitahidi kuwekeza katika misheni na mustakabali wa kanisa Lake.”
Makala asili yalichapishwa kwenye tovuti ya habari ya Lake Union, Lake Union Herald.