West-Central Africa Division

Wanafunzi Kumi Waadventista Waachiliwa Baada ya Kutekwa Nchini Nigeria.

Walionusurika wanasimulia uzoefu wao huku sala na juhudi za jamii zikichangia kuachiliwa kwao.

Nigeria

Abraham Bakari, Picha: Divisheni ya Afrika Magharibi-Kati
Wanafunzi Kumi Waadventista Waachiliwa Baada ya Kutekwa Nchini Nigeria.

Picha: Divisheni ya Afrika Magharibi-Kati

Kama jibu la maombi, wanafunzi kumi Waadventista, wakiwemo kiongozi wa kanisa, waliachiliwa huru tarehe 18 Aprili, 2025, baada ya kutekwa nyara siku mbili kabla na watu wanaoshukiwa kuwa wafugaji wenye silaha kando ya Barabara ya Benin-Okada katika Jimbo la Edo, kusini mwa Nigeria.

Wanafunzi hao walikuwa wakisafiri kutoka Port Harcourt kwenda Chuo Kikuu cha Babcock kuhudhuria programu ya Kongamano Kuu la Vijana (GYC) la Afrika walipovamiwa na watu wenye bunduki kwenye Barabara Kuu ya Benin-Lagos karibu na Ore majira ya saa 11 jioni tarehe 16 Aprili.

Augustin Jika Oka, katibu mtendaji wa GYC Afrika Magharibi, anakumbuka kila tukio, “Tulikuwa tunaimba tukiwa kwenye basi. Tulikuwa na nyakati za msukumo wa kiroho. Kisha tukawapa mapumziko. Haikupita dakika tisa baada ya kusimama, tukasikia milio ya risasi kutoka kushoto na kulia. Tulilala kwenye basi. Walikuja na kutuambia tubebe mizigo yetu midogo.”

Aliendelea, “Tulikuwa 18 na walipogundua baadhi yetu ni dhaifu na wamejeruhiwa, waliagiza dereva awapeleke hospitalini. Tukabaki kumi. Watekaji walikuwa saba, na mmoja wao aliagizwa kwenda kuchunga ng’ombe.”

Mwanafunzi mmoja, Chisaokwu Amadi, alipata jeraha la risasi kutokana na risasi iliyopotea na alikimbizwa hospitalini. Goodluck Blessing, aliyekuwa ameketi karibu naye, alinusurika kutekwa. Alisema ingeweza kuwa yeye.

Goodluck Blessing anashiriki uzoefu wake.
Goodluck Blessing anashiriki uzoefu wake.

“Ilitokea kwamba dakika kumi kabla ya tukio hili, tulibadilishana viti. Ilikuwa ni mshtuko kwangu. Nilikuwa nimekaa karibu na mtu ambaye tayari amepigwa risasi. Damu ilikuwa imenigubika. Nilikuwa pale, nikiwa sina msaada. Kila kitu kilionekana kama sinema.”

Mwanafunzi aliyejeruhiwa alipelekwa Hospitali ya Mafunzo ya Ondo, ambako baadhi ya wenzake walitoa damu ili aokolewe. Kwa sasa anapata matibabu katika Hospitali ya Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Babcock na anaripotiwa kuwa katika hali thabiti. Afisa wa polisi aliyejeruhiwa wakati wa uokoaji pia anapata nafuu.

Kati ya wanafunzi 18, kumi walitekwa nyara. Mateka hao, akiwemo David Jonathan Jr., mkurugenzi wa Huduma ya Kampasi za Umma (PCM) wa Misheni ya Port Harcourt Magharibi, walipelekwa msituni, wakalazimishwa kutembea bila viatu kwa zaidi ya saa 40, kuvuka mito mingi, na kuishi kwa kula maembe, kakao na maji machafu.

David Jonathan, Jr., Mkurugenzi wa Huduma za Kampasi za Umma wa Misheni ya Port Harcourt Magharibi, anashiriki uzoefu wake.
David Jonathan, Jr., Mkurugenzi wa Huduma za Kampasi za Umma wa Misheni ya Port Harcourt Magharibi, anashiriki uzoefu wake.

Alisema, “Wakati fulani tulidhani tutazimia. Lakini Mungu alituma mvua kutupa nguvu. Alitupatia maji na maembe.”

Augustin Jika, akiwa na machozi, alionyesha udhaifu wake.

“Moja ya nyakati za kuhuzunisha zaidi wakati wa utekaji wetu ilikuwa ni pale rafiki yangu wa Biblia, Solomon, alipopigwa na karibu auawe. Alinitazama nami nikamtazama machoni. Hakuwa hata na mpango wa kuwa hapo. Sikuwa nimemwalika moja kwa moja kwenye GYC, lakini aliona machapisho yangu mtandaoni na akasema, 'Ninapenda kanisa lako. Nataka kumkaribia Yesu—labda nitaanza na GYC.' Ndivyo alivyojiunga nasi kwenye safari hiyo.”

Kwa mujibu wa mashuhuda, wakati Solomon Chimbiko, rafiki ambaye si Mwaadventista, alipokaribia kuzama alipokuwa akivuka mto, alimwangalia Jika na kuuliza mara kwa mara, "Je, tutatoka hapa tukiwa hai?" Rafiki yake alijibu kila mara, "Ndiyo, kwa sababu naamini Mungu."

Chimbiko alitambua mujiza wa Mungu katika safari iliyoleta mabadiliko.

"Katika utafutaji wangu wa ukweli, niliamua kuanza safari hii. Tulipokuwa tukimba, nilifikiri itakuwa safari nzuri." Kisha ikaja hali ya kutisha. "Walitupeleka kwenye safari ndefu zaidi niliyowahi kuwa nayo maishani mwangu. Ilibidi tutupe vitu vyetu ili tuweze kuishi. Mtu mwenye sura ya hasira alielekeza bunduki yake kwangu mara tatu. Ilikuwa ni hali ya kutisha. Tulifika kwenye kambi fulani ambapo walitufunga macho. Wakati huo, hakuna kilichoweza kutusaidia. Ni Mungu pekee ndiye aliyetuweka salama. Na alifanya hivyo. Ni wakati wa uamsho kwangu."

Augustin Jika Oka.
Augustin Jika Oka.

Baadhi yao walithibitisha kuwa tukio hilo limeimarisha imani na uaminifu wao kwa uongozi wa Mungu. Wengine, ambao bado wameathirika kisaikolojia, hawakuweza kusema neno. Ingawa kuachiliwa kwa washiriki hao waliotekwa kumeleta faraja kubwa, wahalifu bado hawajakamatwa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Misheni ya Port Harcourt Magharibi, Okey Onwugbonu, “Maombi ya watu wa Mungu yalijibiwa kwa njia ya ajabu. Hakuna kati ya waathirika aliyejeruhiwa zaidi ya mshtuko waliopitia. Mungu alitumia juhudi za Polisi wa Nigeria, Kikosi cha 3rd cha Jeshi la Nigeria, pamoja na wawindaji wa eneo la Warri na walinzi wa jadi ambao walichangia pakubwa katika kuhakikisha kuachiliwa kwao.”

Kufuatia tukio hilo, Rais wa Konferensi ya Yunioni ya Magharibi mwa Nigerian, Ezekiel Adeleye, na Rais wa Yunioni ya Mashariki mwa Nigeria, Bassey Udo, walitoa shukrani kwa Mungu na washiriki wa kanisa duniani kote kwa maombi yao, ambayo yalichangia sana kuachiliwa kwa wanafunzi hao.

Ugochukwu Elem, Mkurugenzi wa PCM wa Divisheni ya Afrika Magharibi-Kati, pia alitoa shukrani, akisema, “Mungu akiwa pamoja nawe, hauko peke yako. Endelea tu kufanya kazi ya Mungu.”

Kongamano la GYC Afrika, lililofanyika kuanzia Aprili 17 hadi 21, 2025, katika Chuo Kikuu cha Babcock, Ilishan-Remo, Jimbo la Ogun, Nigeria, lilimalizika kwa mafanikio. Habari za kuachiliwa kwa wanafunzi hao ziliwaletea washiriki faraja na shangwe kubwa, na viongozi wanasema ilikua hitimisho lenye matumaini kwa kongamano hilo.

Uongozi wa kanisa sasa unalenga kusaidia urejesho wa kihisia na kisaikolojia wa wanafunzi walioachiliwa. Hata hivyo, tatizo kubwa la ukosefu wa usalama nchini Nigeria linaendelea.

Katika ushuhuda wa hivi karibuni, mchungaji kutoka Kaskazini mwa Nigeria alifichua kuwa katika kanisa lake lenye washiriki zaidi ya 100, 44 wanashikiliwa na watekaji nyara kwa sasa.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kati ya Mei 2023 na Aprili 2024, zaidi ya Wanigeria 614,000 waliuawa na zaidi ya milioni 2.2 walitekwa nyara kote nchini. Takwimu kutoka HumAngle Tracker zinaonyesha kuwa katika robo ya kwanza ya 2025 pekee, watu 1,420 waliuawa na 537 walitekwa nyara.

Licha ya hali hii, viongozi wa Kanisa la Waadventista nchini Nigeria wanasema wanaendelea kusimama imara katika maombi, utume, na huduma kwa jamii, wakiamini katika ulinzi na uongozi wa Mungu.

Makala asili imetolewa na Divisheni ya Afrika Magharibi-Kati. Jiunge na Chaneli ya ANN ya WhatsApp kwa sasisho za hivi punde za habari za Waadventista.

Mada