Timu za mawasiliano na AV zikiweka spika kubwa kando ya ufukwe wa Ela huko Port Moresby, Papua New Guinea, usiku wa Ijumaa, Mei 10, zilijaribu vifaa na kumaliza shughuli zao takriban saa kumi alfajiri ya Mei 11, 2024.
Wakati huo, bado ikiwa ni giza la usiku, washiriki wa kwanza wa kanisa la Waadventista Wasabato walikuwa wanafika kwa ajili ya sherehe kubwa ya ubatizo iliyopangwa kuanza saa 1:00 asubuhi. Wengi walitembea kwa maili nyingi, na wengine walitumia magari binafsi, usafiri uliokodishwa, na njia nyinginezo mbalimbali ili kufika mahali pa sherehe mapema.
“Kuna watu 5,000 wanasubiri kubatizwa,” waandaaji walisema, “na lazima tumalize kabla ya saa sita mchana, wakati maji ya bahari yatakapopungua na kufanya ubatizo wa kuzamishwa kuwa mgumu.”
Wakati sherehe ilipoanza, maelfu ya watakao batizwa, washriki wa kanisa, viongozi, na wageni tayari walikuwa wamepanga foleni na kukaa kwenye vizuizi vya mawimbi kwenye pande zote mbili za ufuo. Wachungaji wa kwanza 12 walianza kubatiza huku viongozi wa kanisa wa kikanda wakiwaombea kwa sauti kubwa wale waliokuwa wakijitolea kwa Mungu kupitia sherehe iliyoelekezwa kibiblia. Baada ya masaa machache, wachungaji 48 walikuwa wanabatiza watahiniwa. Ifikapo saa tano asubuhi, sherehe ilikuwa imekamilika kwa kiasi kubwa.
Tukio la Kikanda Lenye Athari za Kidunia
Ubatizo katika bahari ulikuwa mojawapo ya sherehe zilizotia taji siku ya mwisho rasmi ya mfululizo wa injili wa PNG for Christ 2024. Mradi huu uliunganisha juhudi za Adventist World Radio, mpango wa Total Member Involvement, South Pacific Division, na Papua New Guinea Union Mission ya Kanisa la Waadventista, pamoja na mashamba ya makanisa ya kienyeji kushiriki injili kote nchini. Kulingana na waandaaji, wazungumzaji wa kimataifa na kitaifa walihubiri katika zaidi ya maeneo 2,000, yote katika sehemu ya mashariki ya kisiwa cha New Guinea (sehemu ya magharibi ni ya Indonesia) na katika visiwa vingine vya nje vinavyounda PNG.
Mfululizo wa Aprili 26 hadi Mei 11 ulitumika kama “kampeni ya mavuno,” ambapo washiriki walishiriki furaha ya kupokea maelfu ya wanachama wapya baada ya miezi kadhaa ya kuwafikia majirani na marafiki zao kusoma Biblia na kuwaalika kufanya maamuzi kwa ajili ya Yesu. Vyombo vya habari vya umma kama vile redio na televisheni za Waadventista pia viliunga mkono kazi ya mamia ya wachungaji, wanachama wa kanisa la walei, na walimu wa Biblia ardhini.
Ushirikiano wa Logistiki Usio na Dosari
Ubatizo wa Mei 11 kwenye Ufuo wa Ela ulikuwa mojawapo ya sherehe nyingi za kufunga zilizofanyika kwa pamoja lakini huenda ilikuwa kubwa zaidi. Tukio hilo lilihitaji maandalizi makubwa ya kimkakati yaliyohusisha mamia ya viongozi wa makanisa ya kikanda, wachungaji wa makanisa ya kienyeji, wazee, mashemasi, mashemasi wanawake, na wajitolea wengine kwa ajili ya sherehe isiyo na dosari.
Wakati ubatizo ulipokuwa ukiendelea, mashemasi na mashemashai walitoa msaada kwenye ufukwe, wakiwaongoza wagombea kwa mistari mirefu kuelekea kwenye maji. Mashemasi wengine walibaki ndani ya maji, wakiwasaidia watahiniwa kufika kwa wachungaji wanaowabatiza na kuwaongoza kurudi ufuoni. Mashemashai walikuwa wakisubiri ufuoni na taulo na hariri za maua kuwakumbatia wale waliokuwa wakitoka majini.
Upande mmoja wa ufuo, mchungaji alisoma sala kupitia vipaza sauti kila wakati mchungaji aliyeko majini mbali alipoonyesha kwa kuinua mkono wake kwamba alikuwa tayari kubatiza mtahiniwa mwingine. Vikundi vya kwaya kutoka kwa makutaniko ya Waadventista katika eneo hilo walitoa vipengele maalum vya muziki kati kati, ambavyo vilirushwa kupitia vipaza sauti vinavyotumia jenereta kando ya ufuo na zaidi.
“Hii ni karamu ya kiroho,” mwanachama wa kanisa alitoa maoni, “karamu ya kiroho ambayo hatujawahi kuona.”
Baada ya sherehe kukamilika, bado kulikuwa na kazi nyingi za kufanya kwa kikundi kikubwa cha wajitolea.
“Angalau ni siku ya mwisho. Kesho utaweza kupumzika hatimaye,” mmoja wa wageni alimwambia mshiriki wa kanisa la eneo hilo.
“Kesho?” alijibu. “Kesho, tunaanza programu yetu ya kuwahifadhi waongofu wapya!”
Makala asili ilichapishwa kwenye tovuti ya Adventist Review.