Tarehe 12 Aprili, 2025, maelfu ya Waadventista kote Ajentina walijitokeza mitaani kwa lengo moja: kusambaza tumaini kupitia kitabu.
Kama sehemu ya mradi wa kimishonari wa Impacto Esperanza (Tumaini Lenye Athari), Kanisa la Waadventista Wasabato nchini Ajentina liligawa takriban nakala 350,000 za kitabu "The Key to Change", kitabu kinacholenga afya ya akili na ustawi wa kihisia, kilichoandikwa na Bruno Raso na Dkt. Marcelo Niek.

Kwa siku kadhaa kabla ya tukio hilo, ofisi za utawala za viwanja (Fields) na taasisi mbalimbali za Waadventista zilikuwa tayari zimeanza kugawa vitabu.
“Hapa makao makuu ya KOnferensi ya Yunioni ya Ajentina, tulitoka asubuhi ya Ijumaa kwenda Munro madukani katika jimbo la Buenos Aires, tukiwa na vifaa vyetu vyote vya ofisi ili kugawa vitabu. Mapokezi kutoka kwa watu yalikuwa mazuri sana. Nadhani mada ya kitabu ilisaidia sana. Tulipozungumzia afya ya akili, watu walikuwa na mwitikio mzuri sana,” alisema Germán Martínez, mkurugenzi wa Huduma za Uchapishaji.
Kila kiwanja kilisherehekea siku hiyo kwa njia ya kipekee.
“Kwa mfano, timu ya Msheni ya Kaskazini-magharibi mwa Ajentina ilikwenda Hospitali ya Watoto kuwapatia watoto vitabu moja kwa moja. Walitembelea viongozi wa hospitali hiyo na kisha wakazunguka wodi mbalimbali, wakigawa vitabu,” aliongeza Martínez.

Jambo kuu la siku hiyo lilikuwa ushiriki wa washiriki wote wa kanisa, bila kujali umri au idara.
Germán alibainisha: “Watoto, vijana, watu wazima, wazee... wote walijiunga na harakati hii ya kimishonari. Tulipokea picha kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na tukaona kanisa lote likihusika. Idara zote—Pathfinders, Huduma ya Akina Mama, Huduma ya Kibinafsi—pia zilitoka kugawa vitabu.”

Mradi wa Impacto Esperanza haukulenga tu kusambaza ujumbe wa tumaini kupitia vitabu, bali pia kuunganisha kanisa katika utume wa pamoja.
“Ni jambo la kupendeza kuona kanisa likiwa limeungana katika utume. Hatugawi tu vitabu vyenye ujumbe wa wokovu, bali pia tunaimarisha roho ya umoja na huduma,” alisema Martínez.

Zaidi ya hayo, mwaka huu kampeni ilifanyika karibu na siku za kuelekea Pasaka, jambo ambalo lilitupa fursa ya kuwaalika watu kushiriki katika mahubiri maalum yaliyopangwa sehemu mbalimbali za nchi.
"Tulitumia fursa hiyo kugawa mialiko. Wengi waliopokea kitabu pia walialikwa kwenye kituo cha mahubiri karibu na makazi yao kwa ajili ya wikendi iliyofuata," alieleza Martínez.

Harakati hii pia iliripotiwa kwenye vyombo vya habari. Mchungaji José Peñafiel, mkurugenzi wa Nuevo Tiempo Ajentina, alisisitiza ushiriki wa kituo cha redio katika Impacto Esperanza.
“Kila mwaka, Radio Nuevo Tiempo nchini Ajentina huungana na matangazo maalum pamoja na vituo vingine vya redio vya Nuevo Tiempo kutoka nchi mbalimbali za Amerika Kusini ili kutangaza na kufuatilia Impacto Esperanza. Baadaye tunawahoji watu waliopokea vitabu, wale waliotoka kuvisambaza, na watangazaji wetu huandamana na harakati hii kwa matangazo yanayofuatilia kwa karibu matukio ya kanisa zima. Mwaka huu haukuwa tofauti, na Argentina pia iliweza kushiriki katika matangazo haya, ambayo yalirushwa kote Amerika Kusini. Ni furaha kuwa sehemu ya athari hii, kama familia kubwa ya Kanisa la Waadventista ambalo ni Nuevo Tiempo,” alielezea.

Mwishowe, Martínez aliiomba kanisa lote: “Sasa changamoto ni kuomba kwa ajili ya vitabu hivi, lakini zaidi ya yote kwa ajili ya watu waliovipokea. Roho Mtakatifu afanye kazi katika mioyo yao, na wawe wazi kwa ujumbe huu wa thamani.”
Makala asili ilichapishwa kwenye tovuti ya habari ya Divisheni ya Amerika Kusini. Jiunge na Chaneli ya ANN ya WhatsApp kwa sasisho za hivi punde za habari za Waadventista.