Mwezi wa Machi, wamisionari 55 walikusanyika jijini Tokyo, Japani, kwa ajili ya juhudi za wiki moja za kufikia mamia ya maelfu kupitia vipeperushi vienye hadithi za Biblia. Kikundi hiki cha washiriki wa kanisa kilikuja kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Australia, Canada, Marekani, na baadhi ya nchi za Amerika Kusini. Safari ya kimisionari iliandaliwa kwa ushirikiano na Konferensi ya Yunioni ya Japani (JUC) wa Kanisa la Waadventista Wasabato.
Kikundi cha wamisionari kiligawa karibu vijitabu 750,000, ambavyo kwa kawaida hujulikana kama vipeperushi vya GLOW (Giving Light to Our World) tracts. Vijitabu hivyo, vilivyochapishwa kwa lugha ya Kijapani, viliandikwa na kutengenezwa na idara ya Uchapishaji ya Konferensi Kuu. Vilijumuisha mada kama wokovu, afya, uumbaji, na kupata maana ya maisha—mada ambazo JUC ilitambua kuwa muhimu kwa wakazi wa Tokyo.
Kila siku, wamishonari walikuwa na mradi wa kibinafsi wa kutoa trakti 3,000. Vipeperushi vidogo, kwa sehemu kubwa, viliwekwa katika nyumba za watu kupitia masanduku yao ya barua. Kazi hii iliyoonekana kuwa rahisi ilikuwa na changamoto nyingi.
"Wengi wetu tulizoea kutembea kwa wastani hatua elfu ishirini hadi thelathini kwa siku, lakini Jumanne moja yenye mvua ilileta changamoto kubwa," mfanyakazi wa kujitolea Catherine Ge alisema. “Soksi zenye unyevunyevu, trakti za GLOW zenye unyevunyevu, na hali ya hewa ya baridi ilivunja moyo wamishonari wengi, nami pia.”
Safari ya misheni ilikuwa ni muendelezo wa juhudi za kimataifa za kila mwaka ambazo zimekuwa zikiongozwa kihistoria na Konferensi ya California ya Kati ya Waadventista Wasabato, ambapo huduma ya trakti ya GLOW ilianzia. Ingawa juhudi za usambazaji wa vipeperushi 750,000 nchini Japani mwaka huu zilikuwa za kiasi ikilinganishwa na vipeperushi milioni tatu vilivyosambazwa nchini Bolivia mwaka jana, safari ya misheni ya Japani inawakilisha juhudi za kufikia watu katika eneo kubwa la kilimwengu na ambalo halijafikiwa. Kazi hiyo tayari imetoa matokeo ya kutia moyo, kulingana na Yasunari Urashima, Mkurugenzi wa Huduma za Vijana, Uchapishaji, na Vyombo vya Habari wa JUC.
"Konferensi ya Yunioni ya Japani inashukuru sana timu ya misheni ya GLOW kwa huduma yao ya kujitolea huko Tokyo," Urashima alisema. “Kutokana na huduma yao, ‘VOP Online,’ ambayo ni tovuti ambapo Kituo cha Uinjilisti wa Kidijitali (Digital Evangelism Center) cha JUC kinatoa mafunzo ya Biblia mtandaoni, ilikuwa na wageni mara nne hadi tano zaidi ya kawaida wakati wa usambazaji. Pia, kumekuwa na watu waliojiandikisha mara nne hadi tano zaidi kwa ajili ya kujifunza Biblia mtandaoni.”
Takwimu kutoka uwanjani hazikuwa matunda pekee ya uhamasishaji. Kwa mfano, wajitoleaji waligundua kuwa kwa mfano, kwamba maofisa wa usalama katika baadhi ya majengo waliacha kuzuia usambazaji wa trakti katika vyumba vya ghorofa na kuwa wamishonari wenyewe na kusaidia kuzitoa. Baadhi ya wakazi walichukua vipeperushi vya ziada kuvigawa kwa marafiki zao, ikiwa ni pamoja na mchungaji wa kanisa la eneo hilo ambaye alisema alitaka vipeperushi kuvigawa kwa waumini wake. Wengine waliguswa sana na kupokea maandiko ya kiroho kiasi cha kububujikwa na machozi walipoyapokea.
Wakati safari ya misheni ilipofikia tamati, washiriki wengi walieleza shukrani zao kwa ukuaji wa kiroho walioupata.
“Kwa kweli, sikutarajia safari hii ya misheni kuwa hivi,” alisema Erica Mendez. “Nilidhani tutagawa tu vijitabu na ndio basi, turudi nyumbani mara moja. Kile nilichokipata kutoka safari hii ya GLOW kilikuwa tofauti na mapumziko yoyote au safari ya misheni niliyowahi kushiriki hadi sasa. Nilijisikia kama sisi sote ni familia, kama nilivyopata kujionea mbinguni itakavyokuwa pamoja na ndugu zangu na dada zangu katika Kristo.”
“Ninapotafakari juu ya uzoefu huo, niligundua kwamba Mungu ameniongoza mara kwa mara kupitia mateso madogo ambayo ni sehemu ya kazi Yake ya kuimarisha imani yangu na kumtegemea Yeye,” Ge alisema.
Urashima alielezea mipango ya miradi zaidi ya usambazaji wa vipeperushi nchini Japani, iliyohamasishwa na safari ya Machi, ikiwa ni pamoja na Mkutano wa Huduma za Akina Mama huko Kyoto mwezi Aprili na mkutano wa kimtandao wa uinjilisti utakaofanyika na Kituo cha Uinjilisti wa Kidijitali cha JUC mwezi Juni.
Safari za misheni ya fasihi na wamisionari kutoka kote ulimwenguni zitaendelea kutokea, waandaaji walisema. Safari ya usambazaji wa trakti milioni moja imeratibiwa Paris wakati wa Michezo ya Olimpiki wa majira ya joto ya 2024, na Redio ya Dunia ya Waadventista na Idara ya Uchapishaji ya Konferensi Kuu inaandaa mipango mingine ya kupanua zaidi fursa hizi kufikia mamilioni kupitia bidhaa ndogo za vitabu.
Makala haya imetolewa na Adventist Review.