Katikati ya eneo la msitu wa kaskazini ya San Martín, Peru, kuna hadithi ya imani, huduma kwa wengine, na upendo wa Kristo wa Mary Tarrillo Silva, msichana mwenye umri wa miaka 15 ambaye amevutia jumuiya yake kwa kujitolea kwake kwa umisionari.
Silva anakabiliwa na changamoto za kila siku za upatikanaji mdogo wa usafiri na umbali mrefu kuhudhuria shule ya sekondari. Hata hivyo, mapenzi yake kwa ajili ya huduma yamemfanya kuwa mwanga wa matumaini kwa wale walio karibu naye.
Kama mshiriki wa Kanisa la Waadventista, Silva amekubali jukumu lake kama mmishonari, akisafiri kila wiki kufikia jumuiya ya "Palestina Mpya." Huko yeye hutoa mafunzo ya Biblia kwa familia 15 ambazo bado hazijafikiwa na injili. Silva pia huwatia moyo wale wanaomsikiliza wazidi kujifunza Biblia.
Kwa sababu hiyo, wakazi wawili wa kijiji anakotolea mafunzo ya Biblia tayari wamepeana maisha yao kwa Mungu kwa njia ya ubatizo, na wengine wanaendelea kujitayarisha na kujifunza juu ya ujumbe wa injili.
"Mary ni mfano wa kimisionari," anasema Josafat Castillo, mchungaji wa mji ambapo kanisa ambalo binti huyo anahudhuria lipo. "Ujasiri wake wa kukabiliana na vikwazo na kujitolea kwake kwa dhati kushiriki ujumbe wa matumaini katika Yesu ni ushuhuda wa tabia yake," anaongeza.
Licha ya changamoto anazokabiliana nazo, Silva ameonyesha azma isiyoyumba katika misheni yake. Hata katika ushiriki wake katika Klabu ya Pathfinder, licha ya umbali mrefu anaosafiri kuhudhuria kila mkutano, yeye huwa daima anashiriki katika shughuli hizo.
"Hadithi ya Mary inatukumbusha kwamba huduma ya kweli haina mipaka ya kijiografia wala vikwazo vya kimwili," anasema Castillo. “Ni heshima kubwa kuwa na mwanamke kijana anayeleta msukumo katika kusanyiko letu,” anaongeza.
Ushuhuda unaotokana na maandishi yaliyochapishwa na Mchungaji Josafat Castillo
Makala asili ilichapishwa kwenye tovuti ya Kihispania ya Divisheni ya Amerika Kusini.