Kote nchini Albania, huduma za watoto zinabadilisha maisha na kuwalea viongozi wa imani wa baadaye — kama ilivyotokea kwa Mchungaji Euxhenia Bregasi na dada yake Restiola. Licha ya kukua katika familia iliyokuwa inapinga dini, dada hao wawili walipata hifadhi katika kanisa dogo la karibu, ambako nyimbo, hadithi na tabasamu vilipanda mbegu za imani ambazo baadaye zingelielekeza kusudi la maisha yao.
Muda mrefu kabla hajawahi kusimama kwenye mimbari, Mchungaji Euxhenia Bregasi alikuwa msichana mdogo mwenye udadisi, akimfuata dada yake mdogo Restiola kuingia kwenye kanisa dogo lililokuwa mtaani. Hawakulelewa katika familia ya Kikristo, imani haikuwahi kujadiliwa, na dini ilikuwa jambo lililokumbatiwa kwa mashaka au kimya. Lakini katika kanisa hilo dogo, lililojawa na nyimbo, tabasamu na hadithi kuhusu Yesu, kitu fulani kilianza kukua ndani yao.
“Naikumbuka bado siku ya kwanza kabisa,” Euxhenia anakumbuka. “Makumbatio, furaha — vilinipita kiasi. Hatukuwa tumewahi kuhisi aina hiyo ya ukaribishoni hapo mbeleni.” Kile kilichoanza kama udadisi wa kitoto kilikua na kuwa ahadi ya dhati. Shule ya Sabato ikawa darasa lao la kiroho. “Ndipo kwa mara ya kwanza nilijifunza kuomba; nilishika Biblia na kuhisi amani,” aliongeza.
Restiola anakumbuka kipindi cha Krismasi cha watoto ambacho kiligusa moyo wake milele. “Sikuweza kuondoa hisia nilizopata pale kanisani. Nilihisi mazingira ya joto, upendo na amani ambayo sikuwa nimeyajua mahali pengine, hata nikiwa na watu wageni.”
Ingawa njia haikuwa rahisi, hasa katika nyumba ambayo imani ilikataliwa vikali, kanisa likawa kimbilio. Wajitolea, walimu na washiriki wengine waliwasimamia, wakaomba nao na kuonyesha upendo wa Kristo. Kupitia maombi, walivumilia. Kwa siri, walijifunza. Hatimaye, wasichana hao walifanya uamuzi uliobadilisha kila kitu: ubatizo.

Mchungaji wa wakati huo, Sérgio Borges, na mkewe, Adriana Borges, waliwafuatilia kwa ukaribu katika safari yao.
“Licha ya changamoto walizokumbana nazo kupata ruhusa kutoka kwa familia yao, walibaki imara. Baba yao hatimaye alikubali, na walibatizwa katika Camporee ya kwanza ya Pathfinder ya Misheni ya Albania (AM),” anakumbuka Borges. “Tangu wakati huo, Mungu ameheshimu imani yao, na tunajivunia sana kuona walivyo leo.”
Miaka kadhaa baadaye, Euxhenia sasa ni mchungaji, na dada wote wawili wanahudumu kikamilifu katika Kanisa la Waadventista. “Yote yalianza kwenye programu ya watoto,” wanasema.
Na hadithi yao siyo pekee.
Mbegu Zinapandwa Albania Leo
Kote Albania, makanisa ya mtaa yanakumbatia nguvu ya huduma za watoto kupanda mbegu za tumaini, kama ilivyofanyika kwa dada wa Bregasi.
Katika Kanisa Kuu la Tirana, watoto husubiri kwa hamu kambi ya majira ya joto ya kila mwaka inayoratibiwa kwa ushirikiano na ofisi ya Shirika la Maendeleo na Misaada la Waadventista (ADRA) nchini Albania. Ikiwa inaingia mwaka wake wa tatu, mpango huu “hautoi michezo na kazi za mikono pekee bali pia nafasi yenye maana ambapo watoto hukua kijamii na kihisia,” anaeleza Delmar Reis, rais. “Wajitolea kutoka Albania na nje hufanikisha hili, wakimimina upendo katika kila jambo.”
Huko Elbasan, jiji la nne kwa idadi kubwa ya watu nchini Albania, milango ya kanisa hufunguliwa kila wiki kwa watoto, wengi wao wakiwa kutoka familia zisizo za Kikristo. Kupitia hadithi za Biblia, nyimbo, michezo na ubunifu, watoto hawa hukutana na Yesu kwa njia zinazowafaa.
“Mikutano hii siyo tu programu; ni fursa za mabadiliko,” anasema Bregasi, ambaye sasa anahudumu Elbasan.
Katika eneo la milima la Korçë, asubuhi za Jumapili zimejaa vicheko na muziki.
“Kwa zaidi ya miaka miwili, watoto wamekuwa wakikutana kwa hadithi za Biblia, muda wa kucheza na hata programu za ubunifu kama MasterChef, ambapo hujifunza kuhusu ulaji bora kwa njia za kufurahisha na shirikishi,” anaeleza Adriel Henke, mchungaji wa eneo hilo. “Wakati wa Krismasi, zaidi ya watoto 200 hupokea zawadi — ishara halisi ya upendo wa Mungu.”

Na katika kijiji cha karibu cha Dishnice, watoto, wengi wao kutoka familia za Kiislamu, hukutana kila wiki kwa furaha ile ile: hadithi za Biblia, nyimbo na michezo.
Natieli Schaffer, Mkurugenzi wa Huduma za Watoto wa AM, anatoa maoni kuhusu programu hizo.
“Mikakati hii yote, mikubwa na midogo, ina lengo moja: kuwasaidia watoto wakutane na Yesu. Siyo kwa maneno tu, bali kwa matendo. Siyo mara moja tu, bali kwa kudumu,” anasema.
Akiwa na uhakika kwamba kinachohitajika ni mbegu tu, Schaffer anahitimisha, “Kama utawahi kujiuliza kama jambo hilo linaweza kuleta mabadiliko, basi fikiria tu kuhusu Restiola na Euxhenia.”
Makala asili ilichapishwa kwenye yovuti ya habaria ya Divisheni ya Trans-Ulaya. Jiunge na Chaneli ya ANN ya WhatsApp kwa sasisho za hivi punde za habari za Waadventista.