Chuo Kikuu cha Waadventista cha Haiti (UNAH) huko Carrefour, Port-au-Prince, nchini Haiti, kimefunguliwa tena wiki nne baada ya watu waliojihami na silaha kuingia katika chuo hicho mnamo Januari 23, 2024.
"Tumefungua milango yetu tena tukimwamini Mungu kwa ajili ya ulinzi kwa sababu tunapaswa kuendelea kuelimisha," alisema Dk. Sénèque Edmond, rais wa UNAH wiki hii. "Vitisho bado vipo, kwa sababu tunajua chochote kinaweza kutokea, lakini Mungu alituepusha."
Wanafunzi wengi walirudi katika chuo kikuu na mabweni, maafisa wa chuo kikuu walisema. "Wachache bado hawawezi kurejea kwa sababu bado wamekwama katika baadhi ya majimbo kote nchini," alisema Edmond.
Kufunguliwa tena kwa chuo kikuu mnamo Februari 21, 2024, kulishuhudia wasimamizi, walimu, wafanyakazi, na wanafunzi wakishiriki katika kipindi cha kitaifa cha kufunga na kuomba cha siku nne kilichoitishwa na Kanisa la Waadventista nchini Haiti. Wanafunzi, walimu, na wafanyakazi walifanya maombi ya pamoja mara kadhaa wakati wa mchana katika ukumbi wa UNAH wakiomba kukombolewa kutokana na vurugu zinazozidi kuongezeka ambazo zimeathiri washiriki wa makanisa, shule, makanisa na taasisi kote Haiti.
Katika taarifa yake kwa washiriki wa kanisa, Mchungaji Pierre Caporal, rais wa Kanisa la Waadventista nchini Haiti, alisema kwamba hawako peke yao na kwamba uongozi wa kanisa unaelewa mateso yao na kwamba Bwana anaweza kusikia kilio na maumivu wanayoyapitia. "Mungu ana mpango kwa kila mmoja wetu, kwa kanisa Lake na nchi yetu ambayo iko katika machafuko," alisema Caporal. "Kaza macho yako Kwake leo zaidi ya hapo awali na uombe Kwake kwa uvumilivu, uthabiti na bidii na imani kwa ukombozi wa nchi."
Mchungaji Caporal aliwaalika washiriki wa kanisa na familia zao kufanya maombi katika nyumba zao, vikundi vidogo vidogo, makanisa, mashule, na taasisi mbali mbali ili kufunga na kuomba kwa ajili ya utunzaji mwororo wa Mungu.
Makanisa ya mitaa kote Haiti yalishiriki katika maombi hayo na kufunga siku ya Sabato, Februari 24.
Rais wa Divisheni ya Inter-Amerika Mchungaji Elie Henry aliwahimiza viongozi na washiriki wa kanisa wakati wa programu ya mtandaoni mnamo Februari 24 kuendelea kusonga mbele hata katika hali ya kutokuwa na uhakika na dhiki na kumtafuta Mungu katika maombi kila siku. "Ninakualika uendelee kutafakari Neno la Mungu, kutafakari wema wake na kusali kwake kila siku," alisema Mchungaji Henry. "Wakati mwingine tulitarajia Mungu ajidhihirishe kupitia mambo makubwa au matukio makubwa katika maisha yetu lakini Mungu huja kwa pumzi ya upole ili kusema nasi," alisema. "Lazima tuelekeze macho yetu kwa Mungu na tutang'aa kwa furaha kwa kuwa Yeye huja ndani ya mioyo yetu kutuliza mateso yetu na kutoa maana na mwelekeo kwa maisha yetu."
Kulingana na Yonel Bissainthe, mkurugenzi wa mawasiliano katika Kanisa la Waadventista la Bethlehem huko Pétion-ville, Haiti, makumi ya washiriki wa kanisa hilo walijaza kanisa hilo ili kusali, kuungama dhambi zao, na kusali pamoja kwa ajili ya uwepo wa Mungu. “Wengi walifurahi sana kuchukua wakati wa kuweka mizigo yao miguuni pa Yesu na waliondoka wakiwa wamehakikishiwa kwamba Mungu angeleta pumziko kutoka kwa jeuri,” alisema Bissainthe.
Marie Carmen Alvarez, muumini wa Kanisa la Waadventista la Shékina huko Port-au-Prince, alifuatilia programu ana kwa ana mtandaoni siku zote nne za kufunga na kuomba. “Mungu pekee ndiye mwenye uamuzi. Hatuwezi kufanya chochote isipokuwa kumtegemea kupitia maombi na kungojea uingiliaji kati wa Mungu kwa maana tunajua kuwa hali hiyo haitadumu milele, "alisema Alvarez. "Ninaamini kwamba Mungu atafanya kazi kwa niaba yetu."
Kwa miezi kadhaa, makanisa ya Waadventista kote Haiti yamelazimika kurekebisha ibada zao hadi asubuhi au alasiri ili kuwaruhusu washiriki kuwa nyumbani kabla ya giza kuingia. Viongozi wa makanisa waliripoti hivi majuzi kwamba makanisa 15 yamefungwa, na zaidi ya waumini 3,500 wamelazimika kuyahama makazi yao.
Akiwahutubia waumini wengi wa kanisa hilo ambao wamefurushwa kwa sababu ya vurugu katika jumuiya zao, Mchungaji Edgar Etienne, mkuu wa Shule ya Theolojia ya UNAH na mchungaji wa kanisa la chuo kikuu, aliwataka kumtegemea Mungu kila dakika ya siku. “Ni lazima tusali ili kufuata mpango wa Mungu kwa maisha yetu,” akasema Etienne. "Ikiwa lazima tukimbie nyumba zetu, ni Mungu ambaye lazima atuonyeshe mahali pa kwenda. Tusikimbie bila Mungu.”
Kuna zaidi ya Waadventista Wasabato 500,000 nchini Haiti. Kanisa la Waadventista linasimamia makanisa na makutaniko 1,330 yanayosimamiwa na Yunioni ya Haiti na konferensi yake moja na misheni nne. Yunioni pia inamiliki hospitali, chuo kikuu, na shule mingi za msingi na sekondari.
This article was published on the Inter-America Division news site.