Wasimamizi wa Chuo Kikuu cha Waadventista cha Haiti (UNAH), huko Carrefour, Port-au-Prince, Haiti, walifunga shughuli za masomo baada ya kundi la watu wenye silaha kuingia chuoni hapo Januari 23, 2024. Tukio hilo lilitokea saa 2:00 asubuhi. na ilidumu kama nusu saa. Maafisa wa chuo kikuu waliripoti kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa. Mamlaka haijaeleza ni kwa nini kundi hilo la wanaume waliingia katika chuo hicho.
Sénèque Edmond, rais wa UNAH, alikuwa chuoni wakati wa tukio na, siku chache kabla, alikuwa amewaarifu wanafunzi na walimu wa kitivo kwamba hakutakuwa na madarasa wiki hiyo kutokana na ghasia zinazozidi kukabili eneo hilo. Chuo kikuu kinaendelea kutoa huduma fulani kwa kutumia wafanyakazi muhimu.
"Tungependa kushukuru kwa dhati jumuiya yetu yote kwa maombi na maneno ya huruma yaliyoonyeshwa nyakati hizi," alisema Edmond. "Msaada wenu na mshikamano wenu umekuwa chanzo cha nguvu na faraja."
Chuo kikuu kimewaondoa wanafunzi wanaoishi kwenye bweni na kuwaagiza wafanye safari kurudi majumbani mwao. Pia, wamewaeleza walimu na wafanyakazi waache kutembelea chuoni. UNAH ina jumla ya wanafunzi 619 waliosajiliwa na walimu 175 waliogawanyika katika programu za shahada ya kwanza na shahada ya uzamili.
Mbali na shule ya msingi na sekondari yenye zaidi ya wanafunzi 1,500 na maprofesa 122, chuo hicho kina duka la kuoka mikate, duka la vitabu la IADPA, kituo cha redio, Hope Media Center, kiwanda cha kutengeneza vitalu, mashine za uchapishaji, kituo cha kutibu maji ya kunywa, na madarasa na vyumba vya kulala vya chuo kikuu, pamoja na huduma nyinginezo.
Ibada na shughuli za kanisa kwenye chuo zilisitishwa mwishoni mwa juma, alisema Edgard Etienne, mchungaji wa kanisa la chuo kikuu. Alisema waumini wa kanisa hilo katika jumuiya zinazowazunguka na nchi nzima wamekuwa wakiiombea hali hiyo. "Tumewahimiza washiriki wetu kuwa waangalifu na kutekeleza imani yao katika maeneo salama karibu na nyumbani," Mchungaji Etienne alisema.
Mgogoro wa kiuchumi na machafuko ya kiraia nchini Haiti umewaweka viongozi wa kanisa na waumini wao katika hali ya tahadhari kubwa na kusali sana, kulingana na viongozi wa kanisa.
Mchungaji Pierre Caporal, rais wa Yunioni ya Haiti na mwenyekiti wa bodi ya UNAH, alisema anashukuru kwamba Mungu analibariki kanisa nchini Haiti, lakini ana wasiwasi kuhusu wanafunzi ambao hawawezi kuhudhuria masomo. "Nina wasiwasi juu ya uendeshaji wa chuo kikuu na taasisi zingine chuoni, hivyo tunaendelea kuomba ya kwamba Mungu aweze kuchukua hatua kulingana na mapenzi yake ili kubadilisha hali hii," alisema Mchungaji Caporal."
Kwa miezi kadhaa, makanisa ya Waadventista katika sehemu mbalimbali za Haiti yamekuwa wakilazimika kurekebisha huduma zao kuwa asubuhi au mapema mchana ili kuwaruhusu waumini kurudi nyumbani kabla ya giza. "Angalau makanisa 15 yamefungwa, na zaidi ya waumini 3,500 wamepoteza makazi yao," aliripoti Mchungaji Caporal. "Katikati ya changamoto zote ambazo kanisa nchini Haiti inakabiliana nazo, waumini wanajaribu kupata njia mpya za kuhubiri Injili. Wanaamini kwamba wakati umefika wa kuhubiri Injili kwa kila mtu kama ilivyoandikwa katika Ufunuo 14:6–12."
Hospitali ya Waadventista na ofisi za ADRA Haiti karibu na chuo kikuu zinaendelea kufanya kazi kwa tahadhari zinazofaa, Mchungaji Caporal alisema.
Yunioni ya Haiti ina washiriki zaidi ya 500,000 wa Waadventista Wasabato, na makanisa na makutaniko 1,330 yaliyopangwa chini ya konferensi moja na misheni nne. Yunioni hiyo inayo hospitali, chuo kikuu, na shule nyingi za msingi na sekondari.
The original version of this story was posted on the Inter-American Division website.