AdventHealth

Teknolojia Mpya ya Ultrasound Inatoa Matumaini Mapya kwa Wagonjwa Wenye Vivimbe vya Ini

Baada ya matibabu kadhaa, ikiwa ni pamoja na mionzi, uondoaji(ablation), na kemikali (chemotherapy), Kristen James anagundua tiba mpya ya kusaidia kutibu saratani yake ya Hatua ya 4.

Teknolojia ya kisasa ya ultrasound inatoa matumaini mapya kwa wagonjwa wenye uvimbe wa ini.

Teknolojia ya kisasa ya ultrasound inatoa matumaini mapya kwa wagonjwa wenye uvimbe wa ini.

(Picha: AdventHealth)

Kirsten James hakuwahi kufikiria kwamba angekuwa katika hatari ya kupata saratani. Kufanya mazoezi siku sita kwa wiki na kufuata lishe kali, alikuwa mfano wa afya.

“Nilikua na afya nzuri kiasi kwamba sikuwa nikienda kwa daktari,” alisema.

Hiyo ilibadilika mwaka 2022. Akiwa na dalili za matatizo ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula ambazo alidhani ni athari za baada ya kujifungua, alienda kwa daktari na aligundulika kuwa na saratani ya hatua ya 4 ya njia ya haja kubwa. Saratani hiyo ilikuwa imeenea kwenye ini lake, ambako vipimo vilionyesha zaidi ya uvimbe 30.

James, ambaye ni mhandisi wa zamani wa programu za kompyuta kwa ajili ya mpango wa ndege za anga anayeishi Rockledge, Florida, Marekani, na mumewe na watoto wake wawili wa kiume waliobalehe, alikuwa na nia ya kupambana na ugonjwa huo. Baada ya matibabu mengi, ikiwa ni pamoja na mionzi, ablation, chemotherapy, na immunotherapy, madaktari wake walimwambia kuwa hawakuwa na chochote kingine cha kufanya.

Ndipo alipogundua chaguo jipya la matibabu linaloitwa histotripsy lililokuwa linatolewa kwa wagonjwa wenye uvimbe wa ini katika AdventHealth Celebration.

“Histotripsy ni ultrasound inayolenga ambayo hutumia gesi katika tishu kuunda 'wingu la mapovu' ambalo huharibu tishu kwa njia ya mitambo,” alisema Andrew Guzowski, MD, daktari wa upasuaji wa ini katika AdventHealth, aliyefanya taratibu hiyo kwa James. “Inaweza kulengwa kwa usahihi na husababisha uharibifu kamili wa uvimbe bila kuathiri tishu zinazozunguka,” aliongeza.

Eneo la matibabu lililoguswa na ultrasound ni takriban saizi ya punje ya mchele, Dr. Guzowski alisema. Yeye huandaa roboti ya upasuaji kugusa maeneo yote ya uvimbe. Wakati wa wastani wa kuharibu uvimbe mzima ni takriban dakika 23, alisema.

“Taratibu zisizoingilia mwili ni matibabu bora kwa utambuzi wowote, na tunapoweza kuharibu uvimbe kwenye ini bila kufanyiwa upasuaji wowote, wagonjwa wanashukuru na wamepata nafuu vizuri,” alisema Dr. Guzowski.

“Upasuaji wa kuondoa sehemu ya ini unahitaji kukaa hospitalini kwa wiki nzima,” aliongeza. “Wagonjwa wa histotripsy watakaa chini ya uangalizi na kurudi nyumbani siku inayofuata,” alibainisha.

Baada ya kukataliwa na mifumo mingine ya afya, James anafurahi kuwa na chaguo jingine katika AdventHealth.

“Watoto wangu ni kila kitu kwangu; kila kitu ninachofanya ni kwa ajili yao,” alisema James, 49, kuhusu uamuzi wake wa kuendelea kutafuta chaguo za matibabu. “Nahitaji kuwepo kwenye sherehe zao za kuhitimu,” anahitimisha.

Makala asili yalichapishwa kwenye tovuti ya AdventHealth.