Tarehe 3 Julai, 2025, Kikao cha Konferensi Kuu (GC) cha Kanisa la Waadventista wa Sabato kilianza rasmi huko St. Louis, Missouri, kwa makaribisho kutoka kwa viongozi wa sasa wa kanisa na ibada ya asubuhi iliyoongozwa na Mark Finley, msaidizi wa rais wa GC.
Finley alifungua ibada yake kwa kuwatia moyo wajumbe na washiriki “waende wakawafanye watu wa mataifa yote kuwa wanafunzi,” akinukuu agizo kuu ambalo Yesu aliwapa wanafunzi wake katika Mathayo 28 kabla ya kurudi mbinguni.
Finley alielezea dunia ambayo Yesu aliishi kuwa “imejaa upagani na nguvu za kijeshi. Taifa lenye mamilioni ya watu waliokuwa tayari kutazama mapambano ya hadi kifo kwa ajili ya burudani tu na waliamini katika nguvu za miungu iliyotengenezwa na mikono ya wanadamu.”
Kulingana na utafiti aliounukuu, Finley alisema kulikuwa na mkristo mmoja kwa kila watu 500,000 katika Milki ya Kirumi ya karne ya kwanza, na inakadiriwa kulikuwa na wanafunzi 120 wa Kikristo tu.
“Katika mazingira yaliyokuwa hayawezekani, Yesu aliwapa wanafunzi wake agizo la kwenda na kufundisha mataifa yote,” alisema Finley.
Akisoma sura mbalimbali za kitabu cha Matendo, aliwasilisha roho ya wanafunzi wa kwanza waliokuwa wakileta ujumbe wa Biblia kuhusu Yesu. Alieleza kuwa kitabu cha Matendo kinaonyesha hadithi ya watu kutoka tabaka zote za maisha waliobadilishwa na Roho Mtakatifu, ambao kisha walienda na kubadilisha ulimwengu.
Wazo hili ndilo lilikuwa kiini cha ujumbe wake. “Roho lazima atubadilishe kwa kina kabla hajabadili dunia,” alisema Finley. “Na kile ambacho Yesu alifanya wakati huo, atafanya sasa.”
Wajumbe walipokuwa wameketi kwenye Ukumbi wa Dome katika Kituo cha America wakitoka pembe zote za dunia, Finley aliwahimiza kila mtu kuomba kumwagwa kwa Roho Mtakatifu kutokee St. Louis katika kipindi cha siku 10 za tukio hilo.
Hiki ni Kikao cha 62 cha Konferensi Kuu (GC) ya Kanisa la Waadventista wa Sabato na kitadumu hadi Julai 12. Kila siku, isipokuwa Jumamosi zote mbili (Sabato), kutakuwa na ibada za asubuhi na jioni, vikao vya shughuli za kanisa, tamasha za muziki, na ripoti za misheni za kimataifa.
Wajumbe watahudhuria vikao vya masuala ya kanisa kila siku kupigia kura sera, uongozi, na mwelekeo wa kimkakati wa kanisa la ulimwengu kwa miaka mitano ijayo, ikiwa ni pamoja na uchaguzi wa rais wa Konferensi Kuu.
Tazama Kikao cha GC 2025 mubashara kupitia Chaneli ya YouTube ya ANN na ufuatilie ANN kwenye X kwa masasisho ya moja kwa moja. Jiunge na Chaneli ya WhatsApp ya ANN kwa habari za hivi punde za Waadventista.