Mnamo Agosti 16, 2024, Hospitali ya Costa do Cacau huko Ilhéus, Bahia, nchini Brazili, ilipitia wakati wa kipekee katika historia yake: kwa mara ya kwanza, mgonjwa wa ulemavu aliyelazwa hospitalini hapo alibatizwa ndani ya kitengo cha hosipitali hiyo. Kanisa la Waadventista Wasabato liliweka bwawa la lita elfu moja katika hospitali hiyo kwa ajili ya sherehe hiyo.
Ubatizo huo ulifanyika baada ya Felipe Santana de Nascimento, 26, kufanya uamuzi uliochochewa na kundi la vijana Waadventista kutembelea hospitali mara kwa mara. Wakichochewa na hali ya wagonjwa, vijana hao wakiandamana na mchunaji wa kanisa la mtaa huo, walianza kutoa msaada wa kiroho na mafunzo ya Biblia kwa wagonjwa, jambo ambalo lilifikia kilele chake kwa Nascimento kuchagua njia mpya ya imani. “Haiwezekani kukutana na Yesu na kutompenda kwa dhati,” kijana huyo alifichua.
Ubatizo
Mchungaji Osvaldo dos Anjos Junior, ambaye alikuwa ameandamana na mgonjwa katika huo mchakato mzima wa kuongoka, aliongoza ubatizo. "Huu ni wakati wa maana sana, kwa mgonjwa na kwetu sote. Inatuonyesha kwamba imani inaweza kuleta mabadiliko na matumaini hata katika hali mbaya zaidi. Tunaishukuru hospitali hii kwa kuruhusu sherehe hii ifanyike, kwa kuheshimu matakwa ya huyu mgonjwa,” alisema Junior.
Maria Lugiane Cunha, mratibu wa Huduma ya Jamii, alisisitiza umuhimu wa utu katika huduma za hospitali, akielezea nafasi ya kiroho katika utunzaji kamili wa wagonjwa. "Tulipopokea ombi la kufanya ubatizo, tulielewa kwamba ilikuwa jukumu letu kuheshimu matakwa ya mgonjwa. Ingawa ilikuwa jambo jipya kwetu, tulishirikiana na timu ya Kanisa la Waadventista Wasabato kuhakikisha kila kitu kinafanyika kwa usalama na heshima," alishiriki.
Mbali na timu ya afya na washiriki wa kanisa, wagonjwa wengine wa hospitali hiyo walishuhudia tukio hilo. Mbali na kutoa faraja kwa mgonjwa aliyebatizwa, sherehe hiyo ilizua hisia za amani na tafakari kwa waliohudhuria. Ubatizo huo unaashiria sura mpya katika historia ya kitengo hicho, ambacho kinathibitisha kujitolea kwake kwa huduma yenye utu na heshima kwa vipengele vya kimwili, kihisia, na kiroho vya wagonjwa wake. “Ubatizo wa Felipe unatengeneza njia kwa wagonjwa wengine wanaotaka kubatizwa kufanya hivyo, hata wakiwa hospitalini,” anasisitiza Lugiane.
Makala asili ilichapishwa kwenye tovuti ya Kireno ya Divisheni ya Amerika Kusini.