Mnamo Aprili 27, 2024, Kanisa la Waadventista Wasabato nchini Albania lilisherehekea maadhimisho yake ya miaka 32. Washiriki kutoka kote nchini walikusanyika huko Tirana, mji mkuu wa nchi, kwa ajili ya programu maalum, iliyokuw na mada: "Jezusi po vjen sërish!" (Yesu anakuja tena!).
Kipindi kilikuwa na shuhuda, nyimbo, na nyakati za kutafakari kwa utulivu historia ya kanisa nchini humo. Ili kuadhimisha kumbukumbu hiyo, wimbo uliotungwa mahususi na kitabu vilitolewa.
Mchungaji Marko Frasheri, mtunzi wa wimbo huo, alisema, “Kusikia kusanyiko lote likiimba wimbo mpya kwa pamoja... ilikuwa moja ya nyakati kubwa na furaha za maisha yangu.”
Sherehe hiyo pia ilikuwa jukwaa la kuzindua kitabu kilichotafsiriwa hivi karibuni cha Dennis Smith, Siku 40 za Maombi ya Kuimarisha Uhusiano Wako na Mungu. Mchungaji Gentian Thomollari (Mkurugenzi wa Huduma za Uchapishaji za Misheni ya Albania) anaamini kuwa kitabu hicho kitakuwa chachu ya uamsho wa kiroho, kikiwasaidia wanachama 'kupitia miujiza ya Mungu kupitia maombi ya uombezi katika makundi madogo, kama makanisa mawili yalivyokwisha kushuhudia.'
Akitafakari kuhusu umuhimu wa maadhimisho hayo, Mchungaji Delmar Reis, rais wa Misheni ya Albania, alisema, “Wakati washiriki wa kanisa na marafiki wanapokusanyika kusherehekea, ni wakati maalum wa umoja na sifa. Pia ni fursa nzuri ya kuunganishwa, tukitafakari jinsi Mungu ameliongoza kanisa hili kwa miaka mingi.”
Klodjana Koleci, mshiriki wa kanisa la eneo hilo, anakubaliana na Reis. “Tulicheka, tuliimba, na tukamsifu Mungu pamoja. Kushiriki meza na familia yangu ya kanisa lilikuwa jambo lenye maana sana. Ilikuwa siku iliyojaa upendo, furaha, na shukrani, na ninajisikia nimebarikiwa sana kuwa sehemu ya tukio hilo.”
Tukiangalia siku zijazo, Misheni ya Albania imeazimia kufanya sherehe hizi ya kumbukumbu kuwa tukio la kila mwaka. Mada ya sherehe ya mwaka huu ililenga Kuja kwa Pili kwa Yesu. Ni mada inayogonga nyoyo za wengi ndani ya Misheni, ikitumika si tu kama ushuhuda wa utambulisho wa kanisa, bali pia kama wito mkubwa kwa washiriki kushikamana na tumaini lao kuu. Reis alisisitiza, “Kanisa letu lilianzishwa na wale waliotazamia kurudi kwa Yesu kwa hamu, na misheni yetu inabaki thabiti - kueneza habari njema kwamba Yesu atarudi hivi karibuni."
Makala asili ilichapishwa kwenye tovuti ya habari ya Divisheni ya Baina ya Ulaya.