Majuma matatu hivi baada ya Kimbunga Helene—na juma moja baada ya Kimbunga Milton—kuikumba Kusini-mashariki mwa Marekani, jitihada za kuwasaidia wakazi walioathiriwa na dhoruba hizo mbili zinaendelea. Huduma za Jamii za Waadventista (ACS) ni mojawapo ya mashirika ambayo yamehamasishwa kusaidia. Maandalizi yao yalianza kabla ya dhoruba kutua, na baada ya dhoruba kupiga, timu za Kujibu Maafa za ACS (ACS Disaster Response, DR) zilitathmini maeneo yaliyoathiriwa ili kubaini ni wapi wanaweza kuhudumia vyema.
Mvua na upepo mkali kutoka Helene ulikumba Amerika ya Kusini-mashariki, na kuathiri vibaya jumuiya ya Carolina kwa mafuriko makubwa na maporomoko ya matope—katika baadhi ya matukio yakiangamiza miji yote. Idadi ya vifo kutokana na Helene imepanda hadi zaidi ya watu 250. Idadi ya vifo kutokana na Milton kwa sasa inasimama zaidi ya watu 20. Zaidi ya watu milioni 3.2 walipoteza umeme kote Florida, Georgia, Carolinas, na kusini mwa Virginia wakati wa Helene. Wengi pia hawana umeme huko Florida huku Milton ukiendelea kuvuma kote jimboni, ukizalisha angalau vimbunga 45 na mawimbi ya dhoruba za rekodi. Umeme unaendelea kurejeshwa katika maeneo hayo, lakini angalau watu milioni 1 bado hawana umeme hadi Oktoba 12, na maelfu ya watu hawana maji ya bomba.
Majimbo yaliyo na uharibifu mkubwa wa dhoruba ni Florida, Carolina Kaskazini, Carolina Kusini, Tennessee, Georgia, na Virginia. Mkurugenzi wa ACS wa Divisheni ya Amerika Kaskazini (NAD) W. Derrick Lea alisema kuwa kufikia Oktoba 9, NAD ACS na Shirika la Maendeleo na Misaada la Waadventista (ADRA) walikubaliana rasmi kuwa ADRA itachangia kifedha kwa juhudi za ACS katika maeneo yaliyoathirika. "NAD na Yunioni ya Kusini zitahakikisha kwamba matumizi ya fedha hizi yanafanywa kama ilivyokusudiwa na tunawashukuru washirika wetu wa Kimataifa wa ADRA kwa msaada wao," Lea alisema. "ACS na ADRA zinaungana kwa misheni moja: kuleta matumaini na ahueni kwa jumuiya zilizoathirika sana katika Kusini-mashariki. ACS inahudumu katika Divisheni ya Amerika Kaskazini na ADRA inafanya kazi duniani kote, lakini wakati wa matatizo makubwa, tunaungana kama chombo kimoja kuhudumia na kuinua wale wanaohitaji."
Lea aliendelea, “Kupitia Yunioni ya Kusini, tutatambua makanisa yatakayotumia ufadhili huo kwa mahitaji ya haraka ndani ya jumuiya hiyo. Msaada huu utahakikisha msaada unatolewa sasa wakati ahueni ikiendelea.”
Timu za ACS DR kutoka konferensi za Yunioni ya Kusini—Georgia-Cumberland, Carolina, Atlantiki Kusini, Kusini-mashariki, Florida, na Mataifa ya Ghuba—zimetumwa katika maeneo yaliyoharibiwa. Timu za ACS kutoka sehemu zingine za nchi zimejipanga pia, ikijumuisha, lakini sio tu, Konferensi ya Kati na Kusini, Konferensi ya Rocky Mountain, na Yunioni ya Pasifiki Kaskazini, ambazo zote zitatuma watu wajitolea kusaidia inapohitajika.
Lea alishiriki baadhi ya ripoti zilizotolewa na viongozi wa ACS katika maeneo yaliyoathiriwa, akiripoti kwamba kufikia Oktoba 4, tovuti za usambazaji na usimamizi wa ghala zinafanya kazi Georgia, Carolina Kaskazini, Florida, na Tennessee. Ripoti za ACS za ndani zimefupishwa hapa chini.
Konfrensi ya Carolina na Konferensi ya Atlantiki ya Kusini
Konferensi hizi mbili zinafanya kazi pamoja kwani eneo lililoathirika ni kubwa mno kwa konferensi moja kushughulikia. "Timu ya kuchapa kazi" ya ACS inadumisha usambazaji wa ACS huko Asheville, Carolina Kaskazini. Walipokea lori la U-Haul la futi 26 kutoka Fayetteville likiwa limejaa vifaa. Walikuwa katika hali ya kusubiri na tayari kusimamia shughuli za ghala na usambazaji mara tu mkataba wa ghala ulipokamilika. Timu mbili za usimamizi wa ghala za ACS ziko Mooresville. Mnamo Oktoba 5, usambazaji wa vifaa ulianza kwenye eneo la Asheville. “Imekuwa baraka sana kutumikia pamoja na watu wengi wa ajabu kusaidia wengine. Katikati ya giza hili kulikuwa na mwanga. Pia imebadilisha maisha ya wale wanaohudumu,” David Graham, mkurugenzi wa ACS wa Konferensi ya Carolina, alisema. Bidhaa zilizotolewa ni pamoja na maji, bidhaa za watoto (fomula, nepi, n.k.), vituo vya kuchajia simu vinavyotumia nishati ya jua, na MREs (milo tayari kuliwa).
Konferensi ya Georgia-Cumberland
Konferensi hio iliombwa awali kuanzisha ghala huko Georgia. Wakati maelezo yalikuwa bado yanakamilishwa kwa ghala, trela mbili za kuoga za ACS zilianza kufanya kazi katika makao yanayoendeshwa na Msalaba Mwekundu wa Marekani huko Valdosta. Waratibu wa konferensi sasa wanasimamia eneo kubwa la usambazaji, na mipango iko katika hatua za mwisho kufungua na kusimamia ghala la mashirika mengi huko Augusta.
Konferensi ya Florida na Konferensi ya Kusini-Mashariki
Kwa kufanya kazi pamoja konferensi hizi zilifungua ghala la mashirika mengi huko Ocala, Florida, kwa ajili ya jimbo. Konferensi hizo pia zinashirikiana kuendesha maeneo manne au matano ya usambazaji makanisani. "Hii itahakikisha kwamba tuna mawasiliano ya moja kwa moja na jumuiya tunayohudumia huko Florida," Lea alisema. “Kama shirika, tunajaribu kuwahimiza viongozi wetu kila mara kuunganisha ghala lolote tunaloendesha na maeneo ya usambazaji yaliyoanzishwa na sisi. Umma unapaswa kujua kwamba Kanisa la Waadventista Wasabato linahudumu moja kwa moja katika jumuiya yao.” Makanisa ni maeneo ya usambazaji wa vifaa—kanisa la Kwanza la Chuo Kikuu na kanisa la Bethany kila mmoja ulipokea magari mawili ya vifaa. Vifaa vilivyotolewa kutoka kwa wanachama wa kanisa vitapangwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya usambazaji katika makanisa haya na mengineyo.
“Shughuli zinaendelea, na ACS itaendelea kuunganishwa na jamii za ndani tunazohudumia mwaka mzima,” alisema Lea. “Tunajivunia kutoa msaada katika maeneo haya tunayoishi, kufanya kazi, na kuabudu. Haja itaendelea kwa miezi mingi, tunashukuru kwa msaada wote na maombi.”
Makala asili ilichapishwa kwenye tovuti Divisheni ya Amerika Kaskazini.