Middle East and North Africa Union Mission

Waadventista huko Dubai Watambuliwa kwa Ushirikiano na Jumuiya

Kwa mwezi mzima, kikundi kilisambaza vifurushi vya chakula ya Iftar 500-600 kila siku.

United Arab Emirates

Romel Sison (Mume wa Nievelyn) akiwa na vifurushi vya Iftar tayari kwa usambazaji.

Romel Sison (Mume wa Nievelyn) akiwa na vifurushi vya Iftar tayari kwa usambazaji.

Kikundi cha wajitolea cha Waadventista huko Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, kilipokea cheti cha shukrani na kutambuliwa kwa ushiriki wao katika mpango wa usambazaji wa chakula wakati wa mwezi mkuu wa Ramadan. Cheti hicho cha utambuzi, kilichotolewa Mei 21, 2024, kilimsifu Nievelyn Sison, kiongozi wa kikundi, kwa kujitolea kwao kwa njia ya kipekee kwenye mpango wa "Ramadan Aman 10", ambao ulihusisha kugawa milo ya kifungua saumu.

Nievelyn Sison akipokea cheti chake cha shukrani na utambuzi
Nievelyn Sison akipokea cheti chake cha shukrani na utambuzi

Saumu ya Ramadhani (Sawm), moja ya nguzo tano za imani ya Kiislamu, ni wakati Waislamu ulimwenguni pote huzingatia sala (Swala), tafakari, na ujumuiya. Wanaamini kwamba katika mwezi huu Qur'ani ilifunuliwa, ikitoa mwongozo wa kiungu na wokovu kwa Waislamu. Kwa mwezi mzima, wao hufunga kuanzia macheo hadi machweo ya jua, wakijizuia kula, vinywaji na tabia mbaya. Kila mwisho wa siku hufungua saumu kwa tende na maji, kisha hufuatwa na sala ya jioni na Iftar.

Kundi la Waadventista kutoka Kanisa la Waadventista Wasabato la Dubai Visayan walikuwa wakiomba kwa ajili ya fursa za kujihusisha na jumuiya yao. Maria, mshiriki wa kanisa, alipendekeza wangeweza kujitolea kusambaza milo ya Iftar wakati wa Ramadhani. Kikundi kilikubali wazo hilo, na washiriki kadhaa walijiandikisha mtandaoni kujitolea.

Hapo awali, ni washiriki wachache tu ndio walishiriki, lakini shauku na uzoefu wao wa kushiriki uliwahimiza washiriki zaidi kujiunga. Punde, vikundi vingine vya Waadventista kutoka Ras Al Khaimah na Fujairah pia vilihusika.

Picha ya pamoja na wajitolea wakati wa mwezi wa Ramadhani
Picha ya pamoja na wajitolea wakati wa mwezi wa Ramadhani

"Kazi iligawanywa katika sehemu mbili ... Kwanza, wajitoleaji wangejaza masanduku ya Iftar, kisha wayasambaze katika makutano makubwa ya barabara jioni ili kuhakikisha kila mtu anapata Iftar inayofaa," alisema Sison.

Kikundi kilijitolea chini ya mpango wa "Ramadan Aman 10", kikiongozwa na Timu ya Wajitolea ya Ataa Hamdan na kudhaminiwa na Mwana wa Mfalme wa Dubai Sheikh Hamdan bin Mohammed bin Rashid Al Maktoum. Walijitolea kwa siku zote 30 za Ramadan. Sison alibainisha kuwa Waadventista walijitokeza zaidi, hasa wikendi ambapo wajitolea wengine walikuwa na majukumu mengine.

Katika mwezi mzima, kikundi kiligawa vifurushi vya chakula ya Iftar kati ya 500-600 kila siku. Pia walipata fursa ya kukutana na wanajamii mbalimbali, waandaaji kutoka Timu ya Kujitolea ya Ataa Hamdan, Polisi wa Dubai, na maafisa waandamizi ambao mara kwa mara walijiunga na wajitoleaji.

Picha ya pamoja wakati wa sherehe ya utoaji tuzo
Picha ya pamoja wakati wa sherehe ya utoaji tuzo

Sison alisimulia tukio la kukumbukwa katika Hospitali ya Dubai ambapo mwanamke alimwendea kwa furaha kubwa na kumshukuru. “Unanishukuru kwa nini?” Sison aliuliza. “Siwezi kusahau tendo lako la ukarimu wa kugawa Iftar wakati wa Ramadan,” mwanamke huyo alijibu.

"Ilikuwa baraka kuona watu wakitutambua na kutuhusisha na wema kwa jamii," Sison alishiriki.

Juhudi za kujitolea pia zilisaidia kumrejesha mshiriki wa zamani wa kanisa ambaye alikuwa ameacha kuhudhuria ibada. Sison alisisitiza umuhimu wa kuwa na maana katika jamii zinazowazunguka na aliwahimiza wengine kutafuta fursa za kuhudumia.

“Ikiwa tunataka kuwa na umuhimu katika jamii zetu zinazotuzunguka, tunahitaji kutafakari kwa makini na kutazama mahitaji yanayotuzunguka, na kuchukua hatua kuyatimiza. Kuna fursa nyingi sana zinazotuzunguka. Natamani sote tushiriki na kushirikiana furaha ya kuhudumia jamii zetu,” alihitimisha Sison.

Makala hii imetolewa na Misheni ya Yunioni ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Subscribe for our weekly newsletter