Kamati ya Utendaji ya Konferensi Kuu (GC) wakati wa Baraza lake la Kila Mwaka mnamo Oktoba 16, 2024, iliidhinisha upangaji upya wa Konferensi ya Yunioni ya Kaskazini mwa Ufilipino (NPUC) kuwa misheni mbili tofauti, ambao utaanza kutekelezwa Januari 1, 2025. Upangaji huu mpya unakuja baada ya ukuaji mkubwa wa ushirika, utoaji wa kifedha, na shughuli za misheni kote katika eneo hilo.
Ilipendekezwa kwa Kamati ya Utendaji ya GC kupanga upya Konferensi ya Yunioni Kaskazini mwa Ufilipino (NPUC) katika Divisheni ya Kusini mwa Asia-Pasifiki (SSD) kuwa misheni mbili tofauti, kuanzia Januari 1, 2025, kama ifuatavyo:
Misheni ya Yunioni ya Ufilipino ya Luzon Kaskazini (Northern Luzon Philippine Union Mission), ikijumuisha Konferensi ya Luzon ya Kati, Misheni ya Mikoa ya Kati ya Luzon, Misheni ya Mikoa ya Milima, Misheni ya Kaskazini-Mashariki mwa Luzon, na Misheni ya Kaskazini ya Luzon. Makao makuu yake yatakuwa mjini Manila, Ufilipino.
Misheni ya Yunioni ya Ufilipino ya Luzon Kusini (Southern Luzon Philippine Union Mission), ikijumuisha Misheni ya Cavite, Misheni ya Kisiwa cha Mindoro, Misheni ya Palawan, Konferensi ya Kati na Kusini mwa Luzon, na Misheni ya Kusini mwa Luzon. Makao makuu yake yatakuwa mjini Lipa, Ufilipino.
Kamati ya Utafiti ya GC ilikutana mnamo Agosti 5-6, 2024, nchini Ufilipino, ikiwa na viongozi kutoka GC, SSD, na NPUC wakihudhuria. Viongozi walishirikiana kwa bidii kuhakikisha kwamba upangaji upya huu utaboresha misheni ya Kanisa, kuongeza ufanisi, na kutoa msaada mkubwa kwa wafuasi wa ndani.
NPUC imepata ukuaji mkubwa wa kifedha katika miaka sita iliyopita, na ongezeko la fungu la kumi la zaidi ya asilimia 62 na sadaka kupanda kwa asilimia 59. Sabrina De Souza, mweka hazina msaidizi katika GC, alisifu mafanikio haya, akibainisha jinsi michango hii inavyoonyesha uaminifu na kujitolea kwa washiriki katika kusaidia misheni ya Kanisa la Waadventista.
Uamuzi wa kugawa NPUC kuwa mashirika mawili tofauti unatokana na mambo muhimu, ikijumuisha fursa za upanuzi wa misheni, kukuza ukuaji wa kiroho, na kuongeza uwezo wa uongozi ndani ya kanda. Aidha, upangaji upya unalenga kuimarisha juhudi za kulea na ufuasi, kuruhusu huduma iliyo na mtazamo wa karibu zaidi na yenye ufanisi katika ngazi ya mitaa. Kwa kuunda yunioni mbili tofauti, kanisa linanuia kushughulikia mahitaji yanayokua ya washiriki na kuboresha msaada kwa mipango inayozingatia misheni.
Rais wa GC, Ted Wilson, alielezea shukrani na faraja kwa yunioni hizi mpya zilizopangwa upya, akisema, "Tunapongeza maeneo haya yote yaliyopangwa upya. Hii inaonyesha maendeleo ya kanisa la Mungu. Mmekuwa na subira ya kipekee, na mnastahili baraka maalum sana. Kama Zaburi 34:8 inavyosema, 'Onjeni mwone ya kuwa BWANA yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.'"
Mbali na kupanga upya NPUC, mashirika mengine kadhaa ya kanda pia yalipendekezwa kupangwa upya. Hizi ni pamoja na KOnferensi ya Yunioni ya Kaskazini mwa Ghana, Misheni ya Yunioni ya Cameroon, Misheni ya Yunioni ya Amerika ya Kusini na Kati, na Konferensi ya Yunioni ya Kusini mwa Ufilipino. Mapendekezo yote yaliidhinishwa, na mabadiliko yanatarajiwa kuanza Januari 1, 2025, ikiashiria awamu inayofuata ya upanuzi wa misheni ya kimataifa ya Kanisa.
Makala ya asili ilichapishwa kwenye website ya Divisheni ya Kusini mwa Asia-Pasifiki.